Header Ads

test

MSICHANA POLAND AOTA AKIKUMBATIANA NA MPENZI WAKE, AAMKA AKIKUMBATIA NYOKA!

 

Katika kisa cha kushangaza kilichotikisa mitandao ya kijamii nchini Poland, msichana mmoja kutoka mjini Krakow, Iga Radkiewicz (19), alipata mshtuko wa maisha baada ya kuamka usiku akiwa amekumbatia nyoka mkubwa, akidhani ni mpenzi wake aliyekuwa kwenye ndoto tamu!

Kwa mujibu wa gazeti la Croatian Times, Iga alieleza kuwa ndoto hiyo ilikuwa ya kuvutia sana, akihisi yupo katika kumbatio la kimahaba na mchumba wake. Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla alipozinduka usingizini. “Niliruka kutoka kitandani nikitetemeka. Nilikuwa naota njozi murua kuhusu mimi na mwanaume wangu, lakini niliposhituka, nikakuta naangaliana macho kwa macho na bonge la nyoka,” alisema Iga kwa sauti ya hofu.

Msichana huyo alieleza kuwa kwa sekunde chache alihisi moyo wake umesimama. “Kidogo nife kwa hofu,” alisema huku akielezea tukio hilo kama la kutisha lakini la ajabu.

Kwa bahati nzuri, nyoka huyo hakuwa na sumu wala madhara yoyote. Wataalam wa wanyama pori walifika na kumkamata, na ilibainika kuwa nyoka huyo alitoroka kutoka katika duka moja la wanyama wa kufugwa jirani na eneo la tukio.

Msemaji wa polisi alithibitisha kwamba nyoka huyo alikuwa akitafuta sehemu ya kupata joto, jambo ambalo linaelezea kwanini alijipenyeza hadi kwenye blanketi la Iga. “Nyoka huyo hakuwa tishio. Ni wa kufugwa na ni mpole,” alisema msemaji huyo.

Kisa hiki kimeacha wakazi wa Krakow na watumiaji wa mitandao ya kijamii midomo wazi, wengi wakisema hawatalala usingizi kitandani kwa amani tena. Kwa Iga, ndoto ya kimahaba iligeuka kuwa jinamizi la kweli – na cha kushangaza zaidi, nyoka huyo alionekana “kupenda kukumbatiana” kweli kweli!

Cha Umbea TV  tutakuletea visa vya kushtua, kufurahisha na kushangaza kila siku – usikose!

No comments