Nahitaji Ushauri Wenu… Maisha Yamenizidia!
Naitwa mama M… ni mwanamke mwenye miaka 47, naishi Katoro – Geita. Naomba ushauri wenu, kwa moyo mkunjufu kabisa, maana nimebeba maumivu makubwa moyoni mwangu kwa miaka mingi sasa, na sasa naona kama mzigo huu unanizidi.
Miaka ya nyuma, nikiwa bado msichana mdogo, niliolewa na kijana mmoja aliyeitwa Masatu. Nilimpenda kwa moyo wangu wote, na tukaishi kama mume na mke. Miaka mitatu baada ya ndoa yetu, tulijaliwa kupata mtoto wa kike. Lakini furaha hiyo haikudumu. Maisha yalianza kubadilika ghafla. Masatu hakuwa yule mwanaume niliyemfahamu awali. Akawa mtu wa pombe, wanawake, ugomvi… na kila siku alizidi kuwa mgeni machoni pangu.
La kushangaza, kila alipofanya kosa, alirudi akilia, akinililia msamaha, na kusema hata yeye hajui kwa nini anafanya hayo mambo. Aliniomba nimfungie ndani, nisiache atoke kabisa ili ajinusuru. Lakini mimi ni nani? Mwanamke wa kawaida tu… ningewezaje kumfungia mume wangu ndani? Tutakula nini? Tutaishije?
Katika kipindi hicho kigumu, jirani yetu Wilbert – mwanaume mwenye familia yake, mke na watoto – alijitokeza kila mara kuniambia maneno ya faraja, kunisaidia hata kwa mahitaji. Alikuwa bega kwa bega na mimi, zaidi ya ndugu wa damu. Mke wake alikuwa kimya tu, kana kwamba hajui yanayoendelea.
Siku moja, moyo wangu uliteleza. Nikakubali mapenzi ya Wilbert. Nikashika mimba. Nilipomwambia, aliniambia nisithubutu kuitoa. Akanisomea hata vifungu vya Biblia… nikaogopa. Nikalea mimba hiyo, na kwa kweli Wilbert alisimama kama baba wa mtoto wangu, kwa kila hali.
Mtoto alipofikisha miaka mitatu, mambo yakabadilika. Ndugu wa mume wangu Masatu walimwita na kumwambia wazi kwamba mtoto si wake. Masatu alianza kuumwa, akawa na msongo wa mawazo. Mwaka haukupita, akafariki. Kama hiyo haitoshi, mwaka mmoja baadaye, mtoto wangu wa kwanza, yule wa kike, naye akafariki kwa ghafla. Nikabaki mimi na huyu mtoto wa Wilbert.
Sasa mtoto huyo amefikisha miaka 18. Badala ya kuwa faraja yangu, amenigeuka. Ananiambia ni muua watu. Eti nilimuua baba yake mlezi na dada yake. Anataka niondoke kwenye nyumba yangu, niwaachie ng’ombe na kila kitu alichonirithisha baba yangu – eti yeye ndio mrithi sasa. Na kinachouma zaidi, ni kwamba yote haya anayafanya kwa kushirikiana na baba yake Wilbert. Wapo pamoja, na hata mke wa Wilbert yupo kimya kana kwamba hawajui chochote.
Sasa naambiwa Wilbert alijua tangu zamani kwamba mimi ni mtoto pekee wa familia yetu, na alikuwa na mpango huu tangu mwanzo… kupitia mtoto huyu anayeitwa wake, anataka kunipokonya kila kitu. Na sasa naogopa… nahisi wakishanitokomeza, hata huyo mtoto wake hatadumu. Moyo wangu una huzuni, na sina wa kumweleza. Nimetengwa, nimechoka, na sijui nifanye nini tena.
Naomba ushauri wenu, ndugu zangu. Naomba msaada kabla sijavunjika kabisa.

Post a Comment